Jumapili 11 Oktoba 2026 - 19:50
Silaha Hatari Zaidi ya Adui ni Kuchochea Migawanyiko na Kudhoofisha Umoja wa Kiislamu

Hawza/ Mjumbe mwandamizi wa Jumuiya ya Wanazuoni wa Kiislamu nchini Lebanon ameeleza kuwa; jambo hatari zaidi ambalo adui analipa kipaumbele ni kushambulia umoja wa Kiislamu na kuibua migawanyiko miongoni mwa wananchi wa mataifa yetu ya Kiarabu na Kiislamu.

Kwa mujibu wa taarifa ya Idara ya tarjama ya Shirika la Habari la Hawza, Jumuiya ya Wanazuoni wa Kiislamu nchini Lebanon ilitangaza katika taarifa yake kwamba, Sheikh Ghazi Hanineh, Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini wa jumuiya hiyo, alishiriki katika kikao kilichoitwa “Uthabiti na Uaminifu”, kwa mwaliko wa Sheikh Maher Hamoud, Mwenyekiti wa Umoja wa Kimataifa wa Wanazuoni wa Muqawama. Kikao hicho kilifanyika katika ofisi ya Sheikh Maher Hamoud, mjini Sidon, kwa mnasaba wa kuadhimisha mwaka wa tatu tangu kuanza Operesheni ya Tufani ya Al-Aqsa, viongozi mbalimbali wa kisiasa na kidini walihudhuria kikao hicho.

Katika hotuba yake aliyotoa kwa niaba ya Jumuiya ya Wanazuoni wa Kiislamu, Sheikh Hanineh alianza kwa kuwasalimu washiriki wa kikao hicho, kisha akasema: “Tufani ya Al-Aqsa ni tukio ambalo siku yake, pamoja na siku zilizotangulia na zile zilizofuata, ni tofauti na siku za kawaida, kuna mashahidi 100,000 ndani ya Palestina, Lebanon, Iran na Yemen, na karibu watu 200,000 wamejeruhiwa katika nchi hizo. Haya yote yametokea ndio maana nasema, na ninarudia kwa uhakika na ili kila mtu asikie: Sisi tumeshinda  kile ambacho adui alikifanya hakikuwa chochote isipokuwa jaribio la kuvunja azma ya ushindi.”

Aliongeza kusema: “Uharibifu uliotokea Ghaza na Lebanon, kuuawa viongozi wa kijeshi, kuuawa wananchi wa Palestina, Lebanon, Iran na Yemen, pamoja na kupoteza watoto wetu wa kiume na wa kike, vijana, wanawake, wanaume na watoto wadogo, yote hayo yalifanywa kwa lengo la kuvunja azma ya ushindi. Hata hivyo, ushindi tayari umepatikana, kwa sababu mradi wa ‘Israel Kubwa’ sasa uko katika hali ya kuchanganyikiwa na kusahaulika, na iwapo mradi wa Israel Kubwa utatoweka, basi, kwa mapenzi ya Mwenyezi Mungu, hata Israel Ndogo nayo itaelekea kutoweka.”

Mjumbe huyo mwandamizi wa Jumuiya ya Wanazuoni wa Kiislamu alisisitiza kwamba; jambo hili linahitaji muda na subira, alisema: “Sisi ni umma wa mashahidi, sisi ni watoto wa vita vya Badr, Uhud, Al-Ahzab, Mu'tah, Ayn Jalut, Hattin na Yarmouk. Sisi ni watoto wa wale wanaume walioturithisha utukufu na heshima, nasi pia tunapaswa kuwarithisha watoto wetu utukufu huo.”

Aidha, Sheikh Hanineh alibainisha kuwa; jambo hatari zaidi ambalo adui analipa kipaumbele ni kushambulia umoja wa Kiislamu na kuchochea migawanyiko miongoni mwa wananchi wa mataifa yetu ya Kiarabu na Kiislamu.

Alisisitiza umuhimu wa kuimarisha zaidi umoja wa Kiislamu na kuimarisha umoja wa kitaifa, ili kuleta mshikamano katika medani ya ndani na kuwaunga mkono wapiganaji wa muqawama. Alisema: “Ni lazima tusimame nyuma ya wapiganaji wa muqawama walioko Ghaza, kusini mwa Lebanon, Iran, Yemen, Iraq na pia Syria. Ninasema kuhusu Syria kwa uhakika, kwa sababu Syria, hata muda mrefu kiasi gani utakapopita, itarejea tena katika hali yake ya utukufu wa zamani, Mwenyezi Mungu akipenda.”

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha